Tanzania na Uganda zimepata mafanikio makubwa kupitia Mikutano ya Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) iliyofanyika Aprili 2017 Arusha, Tanzania na Agosti 2018 Kampala, Uganda.
Mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kusainiwa kwa Mikataba ya Makubaliano tisa ikiwemo Mikataba ya kushirikiana katika uendelezaji wa bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Tanzania hadi Uganda na ushirikiano katika masuala ya elimu na mafunzo iliyosainiwa wakati wa mkutano wa Kampala.
Utekelezaji wa mikataba hiyo umeelezwa kuwa wa kuridhisha na inalenga kurahisisha ukuaji wa uchumi wa nchi hizo ili kutimiza azma ya viongozi wake, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli wa Tanzania na Mhe. Yoweri Museveni wa Uganda ya kukuza biashara kati ya nchi hizo.
Mikataba iliyosainiwa inahusu uendelezaji wa miradi ya miundombinu mbalimbali ikiwa ni pamoja na nishati ya Umeme, barabara hususan za mipakani, bandari, reli na usafiri wa anga.
Kufuatia mikataba hiyo miradi mbalimbali ipo katika hatua tofauti za utekelezaji ikiwemo mradi wa kuzalisha umeme wa Kikagati/ Murongo uliopangwa kukamilika mwaka 2020. Aidha, kufuatia kusainiwa kwa mkataba wa masuala ya anga katika mkutano wa Arusha mwezi Aprili 2018, Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) imepata fursa ya safari za ndege zake moja kwa moja kutoka Dar Es Salaam hadi Entebbe.
Miradi mingine ni ya ukarabati wa bandari za Port Bell na Bukasa na ukarabati wa meli za Kagawa na Pamba kwa upande wa Uganda ambayo italeta muunganiko mzuri katika usafirishaji hasa baada ya Reli ya Kisasa ya kiwango cha kimataifa inayojengwa na Tanzania itakapokamilika.
Wakati wa mkutano wa Kampala, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb) na mwenzake wa Uganda, Mhe. Sam Kutesa walisisitiza umuhimu wa Serikali za Tanzania na Uganda kuwekeza ipasavyo katika ushoroba wa kati ili kuleta muunganiko kwa ajili ya kukuza biashara. Aidha. Walisisitiza umuhimu wa kuondoa vikwazo visivyo vya kibiashara na kushughulikia changamoto za mipakani kwa haraka kadri zinavyojitokeza.
Kutokana na umuhimu wa utekelezaji wa miradi inayoafikiwa katika mikutano hiyo, pande zote mbili ziliwakilishwa na viongozi wa ngazi ya juu wakiwemo Mawaziri na Makatibu Wakuu.
Kwa upande wa Tanzania, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi. Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwele, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Subira Mgalu walishiriki mkutano huo.
Chanzo: Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Tanzania
