Tarehe 20 Oktoba 2023, Ubalozi ulifanya mkutano na Viongozi wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Tanzania nchini Uganda (TSAU). Lengo la Mkutano huo lilikuwa ni kujadiliana changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo wanafunzi wakiwa nchini Uganda; pamoja na kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kufuata sheria, taratibu na miongozo iliyowekwa na Serikali ya Jamhuri ya Uganda.
Ubalozi uliwashukuru viongozi wa TSAU na wanafunzi wa Tanzania kwa ujumla kwa mchango wao mkubwa katika kuitangaza vyema Tanzania nchini Uganda kupitia ushiriki wao katika masuala mbalimbali yakiwemo: ufunguzi wa vilabu vya Kiswahili katika vyuo mbalimbali nchini Uganda; matamasha ya Utamaduni yanayofanyika vyuoni kwao; kujitokeza kwa wingi kushangilia timu mbalimbali kutoka Tanzania zinapokuja Uganda kwenye mashindano ikiwemo Ligi ya Mabingwa CAF kwa Wanawake kuwania uwakilishi wa Kanda ya CECAFA yaliyofanyika kuanzia tarehe 12 Agosti 2023 hadi tarehe 30 Agosti 2023.
Vilevile, Ubalozi ulitoa taarifa kwamba Serikali ya Tanzania imeanzisha rasmi Mfumo wa Kidijitali wa kuwasajili diaspora wenye asili ya Tanzania (diaspora digital hub). Kupitia mfumo huo, wanafunzi wa Tanzania wanaosoma nje ya nchi wanaweza pia kujisajili. Hivyo, Ubalozi uliwashauri wanafunzi hao kutembelea mfumo huo ili na wao pia waweze kujisajili.
Aidha Bw. George Madaraka, Rais wa Jumuiya ya TSAU aliushukuru Ubalozi kwa kutenga muda wa kuonana na kufanya mazungumzo nao na pia kwa ushirikiano mkubwa wanaopata mara wanapohitaji huduma Ubalozini.
Mwisho, Ubalozi uliwasisitiza wanafunzi kujidhatiti katika masomo yao na kuhakikisha kuwa wanapata ufaulu mzuri kwa kuwa ndicho kitu cha msingi kilichowaleta nchini Uganda. Ubalozi uliendelea kuwakumbusha kuwa Ubalozi ni nyumbani kwa Watanzania wote na hivyo wasisite kuwasiliana nao pale wanapohitaji ufafanuzi wowote.

