Tarehe 23 Machi, 2024, Ubalozi uliandaa mkutano na diaspora wa Tanzania wanaoishi Uganda. Mkutano huo ulifanyika katika viwanja vya Ubalozi vilivyopo jijini Kampala. Lengo la mkutano huo lilikuwa ni kumtambulisha Mhe. Meja Jenerali Paul Kisesa Simuli, Balozi mpya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Jamhuri ya Uganda. Mhe. Balozi alianza rasmi kutekeleza majukumu yake nchini Uganda tarehe 5 Machi 2024.
Diaspora walipata fursa ya kumkaribisha Mhe. Balozi na kuahidi kuendelea kushirikiana na Ubalozi katika kutekeleza majukumu yake. Kwa upande wake, Mhe. Balozi aliwashukuru pia Diaspora hao kwa mapokezi mazuri na kuahidi kushirikiana nao. Aliwasihi pia kuendelea kuikuza lugha ya Kiswahili inayoendelea kuwaunganisha Watanzania popote pale walipo duniani.
Sambamba na hilo Ofisi ya Ubalozi iliweza kutoa ufafanuzi wa masula mbalimbali ambayo yaliibuliwa na Diaspora. Vilevile, ulitumia mkutano huo kuzinadi fursa ambazo Watanzania wanaweza kuzitumia wakiwa Uganda ikiwemo matumizi ya bandari za Tanzania kwa ajili ya kusafirisha mizigo yao na kutumia ndege za Shirika la Ndege la Tanzania ambalo linafanya safari zake kati ya Tanzania na Uganda. Aidha, Ubalozi ulihamasisha Diaspora wasaidie kuzitangaza fursa hizo ili ziweze kutumiwa na wadau mbalimbali waliopo nchini Uganda kwa lengo la kuchochea uchumi wa nchi yetu.


