Tarehe 1 Desemba 2023, Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uganda ulifanya mkutano na baadhi ya viongozi wa vilabu vya Kiswahili katika vyuo vikuu nchini Uganda. Lengo la mkutano huo lilikuwa ni kujadiliana changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo katika kuendesha Vilabu vya Kiswahili; kufanya tathmini ya Vilabu hivyo na kujadiliana masuala mbalimbali kuhusu kuendeleza lugha ya Kiswahili nchini Uganda. 
 
Ubalozi ulitumia fursa hiyo kuwahimiza wanafunzi hao ili waendane na kasi ya Serikali ya Uganda ya kusambaza Kiswahili nchini Uganda. 
 
Ufunguzi wa vilabu vya Kiswahili katika vyuo vikuu ni mpango ulioanzishwa na Ubalozi mwaka 2021 ikiwa ni miongoni mwa mikakati ya kukuza Kiswahili nchini Uganda kupitia Vyuo Vikuu. Hadi sasa, Vyuo vilivyofungua Klabu za Kiswahili ni pamoja na Chuo Kikuu cha Bugema; Chuo Kikuu cha Makerere, Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala (Makao Mkuu na Kampasi ya Ishaka); Chuo Kikuu cha Kampala; na Chuo Kikuu cha Mbarara.