Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Jamhuri ya Uganda kwa kushirikiana na Shirika la Uvuvi la Ziwa Viktoria la Jumuiya ya Afrika Mashariki (LVFO) liliopo Jinja, Uganda uliandaa ziara ya mafunzo ya ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba kwa wafugaji wa samaki na Maafisa kutoka Mkoa wa Mwanza. Ziara hiyo ilifanyika kuanzia tarehe 10 hadi 12 Agosti 2022, katika maeneo ya Kajjansi na Jinja nchini Uganda. Ujumbe huo uliweza kutembelea Kituo cha Utafiti wa Ufugaji Viumbe Maji cha Kajjansi kilichopo chini ya Taasisi ya Utafiti wa Rasilimali za Uvuvi nchini Uganda (NAFIRRI); LVFO; Yalelo Fish Farm Uganda; Source of Nile Farm; na Masese Cage Fish Farmers Co-operative Society. 

Ziara hiyo ilitoa fursa nzuri kwa ujumbe wa Tanzania kujifunza na kubadilishana uzoefu katika ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba na jinsi ya kutengeneza chakula cha samaki. Ujumbe ulinufaika na elimu katika uzalishaji wa vifaranga bora vya samaki; lishe bora ya samaki hasa utumiaji wa nzi chuma (black soldier fly) kama mbadala wa matumizi ya dagaa; matumizi ya dawa za mimea asili kwa samaki; namna bora ya utengenezaji wa vizimba; ufugaji wa kibiashara unaohusisha jamii yaani vyama vya ushirika; na masoko mbalimbali ya bidhaa za samaki. 

Ujumbe huo ulipata nafasi ya kufanya mazungumzo na Mhe. Dkt. Aziz P. Mlima, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Jamhuri ya Uganda ambaye alitoa rai kwa wafugaji na wadau wa sekta ya uvuvi kutumia maarifa hayo waliyojifunza katika kusambaza elimu, kuboresha na kukuza uzalishaji wa samaki kwa njia ya vizimba nchini Tanzania.