Ubalozi uliandaa ziara ya mafunzo ya ufugaji kwa wafugaji kutoka Mkoa wa Kagera yaliyofanyika kuanzia tarehe 23 hadi tarehe 25 Juni 2022. Mafunzo hayo yalifanyika kwa njia ya nadharia na vitendo katika shamba la Mutanoga lililopo Rushere; na Temupe lililopo Lyantonde. Mashamba hayo yapo eneo la Mbarara, Magharibi mwa nchi ya Uganda. 

 

Ziara hiyo ilitoa fursa nzuri kwa ujumbe wa Tanzania kujifunza na kubadilishana uzoefu katika ufugaji wa biashara wa ng’ombe wa nyama na maziwa. Ujumbe ulinufaika na elimu katika uzalishaji wa ng’ombe kwa kutumia mbegu bora; lishe bora ya mifugo; upandaji wa nyasi; kuhifadhi chakula cha mifugo; namna bora ya usimamizi wa mifugo kwa kuzingatia mabadiliko ya misimu ya mwaka; ufugaji endelevu kutoka kizazi kimoja kwenda kingine; na uchangiaji katika maendeleo ya familia na jamii.