Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alifanya Ziara ya Kikazi nchini Uganda tarehe 17 na 18 Desemba 2022. Mhe. Waziri Mkuu alimwakilisha Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye sherehe za Kumbukizi ya miaka 75 ya Kujengwa msikiti wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Makerere na miaka 50 ya Jumuiya ya Wanafunzi wa Kiislamu ya Chuo Kikuu cha Makerere (MUMSA) zilizofanyika tarehe 17 Desemba, 2022 katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Makerere.
Msikiti huo ulijengwa mwaka 1947 kwa ufadhili kutoka Chuo Kikuu cha Makerere kwa kushirikiana na Serikali ya Zanzibar chini ya Mfalme Adulla. Mfalme Abdulla aliufungua msikiti huo mwaka 1948 alipofanya ziara yake ya kwanza rasmi katika Chuo hicho.
Wakati wa hotuba yake, Mhe. Waziri Mkuu aliahidi kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kuenzi uhusiano na ushirikiano wa kidini na kiutamaduni uliopo kati ya nchi hizi mbili.
Wakati wa ziara hiyo, Mhe. Waziri Mkuu alipata pia nafasi ya kufahamu fursa mbalimbali zilizopo nchini Uganda ambazo Watanzania wanaweza kunufaika nazo kama vile ufugaji wa kisasa wa ng’ombe wa nyama na maziwa; na ufugaji wa samaki wa vizimba.