Maonesho ya 22 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) maarufu kama “Juakali” yalifanyika katika viwanja vya Kololo kuanzia tarehe 8 hadi 18 Desemba, 2022. Maonesho hayo yaliyoongozwa na kauli mbiu “Nunua Bidhaa za Afrika Mashariki, ili kujenga Uchumi Stahimilivu na Endelevu wa Afrika Mashariki” yalilenga kutoa fursa kwa Wajasiriamali Wadogo na Wakati zaidi ya 1,500 kutoka katika Nchi zote saba za EAC kuonesha huduma na bidhaa mbalimbali wanazozalisha na kubadilishana uzoefu, ujuzi, na taarifa baina yao; sambamba na kukuza na kupanua wigo wa masoko mapya. 

 

Wajasiriamali zaidi ya 200 kutoka Tanzania walishiriki kwenye maonesho na kupata fursa ya kuonesha bidhaa, huduma na fursa zinazopatikana nchini Tanzania. Bidhaa walizozionesha ni kama vile mavazi ya asili, bidhaa za baharini, bidhaa za kilimo zilizoongezewa thamani, mashine za kuzalisha bidhaa mbalimbali, madawa ya asili, vito vya thamani na madini, utalii, na bidhaa za ngozi kama vile viatu, mabegi na mikoba. Mbali na kutangaza bidhaa hizo, wafanyabiashara hao waliweza kutengeneza mtandao wa kuweza kuuza bidhaa zao kwenye nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

 

Ubalozi kwa kushirikiana na Maafisa wa Serikali Kutoka Tanzania waliweza kutumia fursa ya maonesho hayo kutoa elimu kwa baadhi ya Wajasiriamali kutoka Tanzania kuhusu namna bora ya ufanyaji wa Biashara katika masoko ya Uganda. 

 

Kwa upande mwingine, Ubalozi uliratibu diaspora watanzania wanaoishi nchini Uganda kushiriki kwenye maonesho hayo. Diaspora hao walipata fursa ya kujumuika na wajasiriamali kutoka Tanzania kuonesha bidhaa, huduma na fursa zinazopatikana nchini Tanzania.