Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na mwenzake wa Uganda Yoweri Museveni wa wamesaini rasmi mkataba wa utekelezaji wa mradi wa  kujenga bomba la mafuta ghafi kutoka Magharibi mwa Uganda hadi bandari ya Tanga Tanzania.

Hii ikiwa mara ya kwanza kwa rais Samia kufanya ziara rasmi tangu alipoapishwa kuongoza Tanzania, ametimiza mpango huo ulioahirishwa kufuatia kifo cha Rais wa awamu ya tano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.

Ujenzi wa bomba  hilo lenye umbali wa kilomita 1,440 utagharimu dola bilioni 15 za Kimarekani na unatarajiwa kuanza kutekelezwa katika muda wa miezi sita ijayo.

Hii ni baada ya masuala fulani ikiwemo kusainiwa kwa  mkataba wa nchi mwenyeji kati ya Tanzania na makampuni wadau katika mradi huo.

Akizungumza wakati hafla ya utiaji saini rais Samia amesema "ninafahamu vyema kwamba kabla ya utekelezaji wa mradi huu, bado kuna masuala ambayo yanahitaji kushughulikiwa. Kwa hiyo naomba wahusika wote washirikiane kuhakikisha kuwa yanashughulikiwa haraka iwezekanavyo kuhakikisha kuwa mradi huu unaanza mara moja"

Museveni: Mradi huu ni kielelezo cha ushirikiano

Miongoni mwa hatua ambazo zinahitaji kushughulikiwa ni kuwasilishwa kwa muswaada wa utekelezaji wa mradi huo katika bunge za Uganda na Tanzania ili mradi huo utambuliwe rasmi na utekelezwe kisheria.

Katika hafla iliyofanyika ikulu ya Entebbe Uganda, rais Yoweri Museveni ameelezea kuwa hatua ya kusainiwa kwa mkataba huo ni muhimu sana na ya kihistoria kwani itashiria kwamba shughuli za uchimbaji mafuta zinawezae kuanza Uganda baada ya raslimali hiyo kugunduliwa mwaka 2006.

Ameongezea kuwa hatua hii ya kudhihirisha ushirikiano wa kibiashara na Tanzania ni kielelezo kuwa nchi yake iko tayari kujenga mahusiano zaidi kiuchumi na kisiasa na Tanzania.

"Miaka 42 iliyopita, tarehe kama hii ndiyo siku majeshi ya Tanzania ya ukombozi yalipouteka mji wa Kampala na afisa wetu wa kijeshi Oyite Ojok akatangaza kwenye redio ya Uganda kwamba utawala wa Iddi Amin ulikuwa umeng'olewa mamlakani. Kwa hiyo leo ni siku ya ushindi wa aina tatu kwa Tanzania na Uganda" amesema rais Museveni.

Mradi kutekelezwa kwa muda wa miezi 36

Imesadifu pia kuwa siku hii ya tarehe 11 Aprili ni miaka 42 tangu jeshi la ulinzi wa wananchi wa Tazania TPDF iliposaidia kundi la Waganda waliokuwa uhamishoni kumng'oa mamlakani Iddi Amin mwaka 1979.

Mtangulizi wa Samia, hayati Dkt John Pombe Magufuli alikuwa amepangiwa kushiriki katika hafla hiyo tarehe 22 mwezi Machi mwaka huu. Lakini Alipofariki tarehe 17 siku tano kabla ya kufanyika kwake, ilibidi kuhaihirishwa.

Kulingana na ratiba ya utekelezaji wa mradi  huo wa ujenzi wa bomba, shughuli hiyo imepangiwa kukamilika katika kipindi cha miezi 36 baada ya kusainiwa kwa mkataba huo na hapo ndipo uzalishaji wa mafuta ghafi kwa ajili ya biashara utaanza.

Kama ilivyokuwa ada kwake kuhakikisha kuwa miradi inaleta manufaa ya haraka kwa wananchi, Hayati Magufuli alikuwa amependekeza utekelezaji wa mradi huo ujulikanao kama EAPCO wa gharama ya dola  bilioni 3.5 za Kimarekani  ufanyike  katika muda wa miezi 18 tu.

Kwa mujibu wa  muundo wa sasa wa mgawanyo wa hisa, kampuni ya Ufaransa Total itamiliki asilimia 45, kampuni ya China CNOOC asilimia 35, Uganda itamiliki asilimia 15 na asilimia 5 iliyobaki iwe ya Tanzania kupitia kwa kampuni yake ya maendeleo ya mafuta TPDC.

Mwenyekiti na mkurugenzi mkuu wa Kampuni ya Total Patrick Pouyanne amezisifu Uganda na Tanzania kwa kujtolea kuhakikisha kuwa mradi huo unafanyika ukiashiria kuanzishwa rasmi kwa uchumi wa mafuta kanda ya Mashariki mwa Afrika.

Tangu kuanzishwa mpango wa biashara ya mafuta, maazimio kadhaa ya utekelezaji yamekwazwa kutokana na mizozo ya kido kati ya serikali na makampuni yaliyotaka kuwekeza katika sekta hiyo.

  • Rais Samia ashuhudia utiaji saini wa utekelezaji wa mradi ujenzi wa bomba la mafuta ghafi