Tarehe 28 Ocktoba 2022, Kanali Hamza M. Burah, Mwambata Jeshi alimwakilisha Mheshimiwa Dkt. Aziz P. Mlima, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uzinduzi wa Klabu ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala (KIU). Sherehe za uzinduzi wa Klabu hiyo, zilifanyika katika Makao Makuu ya Chuo cha KIU yaliyopo Kasanga Jijini Kampala.
Katika hotuba yake, Kanali Burah aliushukuru uongozi wa Chuo kwa maamuzi yake ya kuanzisha Klabu hiyo katika Chuo cha KIU. Vilevile, aliwashawishi wanafunzi kuitumia Klabu hiyo kama fursa ili iweze kusaidia kukuza matumizi ya lugha ya Kiswahili. Alielezea umuhimu wa matumizi ya lugha ya Kiswahili ambayo inaendelea kuiunganisha dunia hususan Bara la Afrika katika shughuli mbalimbali za kisiasa, kijamii na kiuchumi.