Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Jamhuri ya Uganda umeadhimisha kumbukizi ya miaka 100 ya kuzaliwa kwa Baba wa Taifa, Hayati Julius Kambarage Nyerere. Maadhimisho hayo yalifanyika katika Kituo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo katika Chuo Kikuu cha Makerere tarehe 13 Aprili, 2022.

Ni vyema ikafahamika kwamba Hayati Mwl. Nyerere alipata elimu yake katika Chuo Kikuu cha Makerere. Hali hiyo imesababisha maadhimisho hayo kua na hisia za kipekee nchini Uganda hususan katika Chuo cha Makerere. 

Wakati wa maadhimisho hayo, Mheshimiwa Dkt. Aziz Ponary Mlima, Balozi wa Tanzania nchini Uganda pamoja na wenyeji wake Prof. Barnabas Nawangwe, Makamu Mkuu wa Chuo kikuu cha Makerere na Dkt.  Nansozi K. Muwanga, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uongozi cha Julius Nyerere walipata fursa ya kutembelea chumba alichokuwa akilala Mwalimu Nyerere kipindi akiwa chuoni hapo. 

Maadhimisho hayo yalienda sambamba na maonesho ya biashara ambapo diaspora wa Tanzania wanaoishi Uganda walipata fursa ya kuonesha bidhaa na fursa mbalimbali zinazopatikana nchini Tanzania. 

Katika maadhimisho hayo kulifanyika mdahalo chini ya kaulimbiu “Miaka 100 ya Mwalimu Nyerere: Tumuenzi kwa kudumisha Umoja, Amani na Kazi.”; Wanafunzi kutoka katika Vyuo Vikuu ambavyo vimeanzisha Klabu za Kiswahili walishindana katika mdahalo huo. Vyuo hivyo ni Chuo Kikuu cha Makerere; Chuo Kikuu cha Bugema; na Chuo Kikuu cha Kampala. Chuo Kikuu cha Makerere kilishinda katika mashindano hayo.

Aidha, kulifanyika mashindano ya kuzungumza Kiswahili ambapo wananchi mbalimbali ambao hawajui Kiswahili walifundishwa maneno ya msingi ya Kiswahili na kisha kupewa maswali mafupi kuangalia uelewa wao. 

Pia, Ubalozi kwa kushirikiana na Shirika la Utangazaji Tanzania na Shirika la Utangazaji Uganda ulitoa Tuzo za Kiswahili kwa wadau waliopo Uganda ambao wanachangia katika kukuza matumizi ya Kiswahili nchini Uganda. Wadau waliopewa Tuzo hizo ni Prof. Augustine S.L. Bukenya kwa kutambua mchango wake katika kuandaa itifaki na mitaala ya maendeleo ya Kiswahili katika Vyuo Vikuu vya Uganda; Bw. Monday Geofrey Akol Amazima Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji Uganda (UBC) kwa kutambua mchango wake katika kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili kupitia vyombo vya habari; na Bw. Isaac Mumena Musana, Mtangazaji wa BBC kwa kutambua mchango wake katika kukuza na kutumia Lugha ya Kiswahili katika vyombo vya habari vya kimataifa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kituo cha Uongozi cha Julius Nyerere kilichopo katika Chuo Kikuu cha Makerere, Dkt. Nansozi Muwanga aliishukuru ofisi ya Ubalozi kwa mchango wake katika kufanikisha tukio hilo pamoja na ushirikiano ambao umekua ukitolewa na ofisi ya Ubalozi tangu kuanzishwa kwa Kituo hicho.